IQNA

Jeshi la Israel laua Wapalestina zaidi ya 54 katika maandamano Ghaza

19:01 - May 14, 2018
Habari ID: 3471512
TEHRAN (IQNA)- Wapalestina wasiopungua 54 wameuawa shahidi baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.

Wapalestina wengine zaidi ya elfu mbili wamejuruhiwa katika mauaji hayo ya umati ambayo yanatekelezwa na utawala katili wa Israel. Wapalestina wameitisha maandamano ya leo kwa munasaba wa kukumbuka mwaka wa  70 wa Siku ya Nakba, siku ambayo Wapalestina walitimuliwa kutoka katika ardhi zao za jadi na mahala pao kuchukuliwa na Wazayuni waliounda utawala bandia wa Israel. Aidha mandamano ya leo ambayo ni maarufu kama 'Maandamano ya Haki ya Kurejea", yamefanyika kwa lengo la kulaani vikali na kupinga hatua ya Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi mji wa Quds Tukufu au Jerusalem.

Tokea Machi 30 Wapalestina wamekuwa wakishiriki katika maandamano hayo ya 'Haki ya Kurejea' kila Ijumaa ambapo hadi sasa karibu Wapalestina 50 wameuawa shahidi baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa Israel katika maadanamano hayo ya amani ambayo hufanyika katika mpaka wa Ghaza na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Mnamo Disemba 6 mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza uamuzi wa kuhamisha ubalozi wa nchi hiyo kutoka Tel Avivi hadi Quds Tukufu na uamuzi huo unatekelezwa rasmi kuanzia leo. Uamuzi huo wa Trump ulipelekea kuibuka wimbi kubwa la malalamiko huko Palestina na kufuatiwa na maandamano yanayojulikana kama "Haki ya Kurejea" ambayo yalianza tangu Machi 30 mwaka huu, na yanatazamiwa kuwa makubwa zaidi siku hiyo ambayo Marekani imetangaza kuuhamishia ubaliozi wake Baitul Muqaddas. Tokea Trump atangaze uamuzi wake huo ,wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 120 ambao wamekuwa wakiandamana kwa amani kupinga uamuzi huo.

Siku ya Ijumaa maelfu ya Waislamu na wapenda haki kote duniani walishiriki maandamano ya kupinga hatua ya kiuhasama ya Marekani ya kuuhamishia ubalozi wake katika mji wa Quds Tukufu, kutoka Tel Aviv.

3714401

captcha