IQNA

Sayyid Hassan Nasrallah

Marekani na utawala wa Kizayuni zinachochea vita dhidi ya Lebanon

10:36 - May 03, 2019
Habari ID: 3471939
TEHRAN - (IQNA)-Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema hali katika Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) inaonyesha kuwepo uchochezi unaotekelezwa na Marekani, baadhi ya nchi za eneo na vyombo vya habari ili kuuwezesha utawala wa Kizayuni Kuanzisha vita

Sayyid Hassan Nasrallah Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameyasema hayo Alhamisi Alasiri akizungumza kwa njia ya televisheni katika kumbukumbu ya kuuawa shahidi kamanda mwandamizi wa Hizbullah Shahidi Mustafa Badreddine. Kiongozi wa Hizbullah amesisitiza kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi, Marekani na utawala wa Kizayuni hivi karibuni zimekuwa zikieneza uvumi kuhusu vita dhidi ya Lebanon lengo likiwa ni kuishinikiza Lebanon. Amesema lengo kuu la uvumi huo ni kuifanya Lebanon iliegeze msimamo hasa kuhusu ardhi zake za mpaka wa baharini na Mashamba ya Shebaa.

Kiongozi za Hizbullah ameongeza kuwa, "Israel inafahamu fika kuwa, vita vyovyote dhidi ya Lebanon vinahitaji maamuzi na mahesabu ya kina. Hizbullah ipo tayari kwa ajili ya kujibu chochoko zozote. Utawala wa Kizayuni unaogopa kuanzisha vita vipya hata katika Ukanda wa Gaza, achilia mbali Lebanon."

Amesema bayana kuwa, "Vikosi vyote vya utawala haramu wa Israel vitaangamizwa mbele ya macho ya vyombo vikuu vya habari na dunia yote kwa ujumla iwapo vitathubutu kutia mguu katika ardhi ya Lebanon. Hatuwezi kusalimisha hata shibri moja ya ardhi ya Lebanon."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, "Utawala wa Kizayuni hauna picha ya taathira hasi za mpango wake wa kutaka kulisukuma eneo katika vita. Hawajui nini kinachowasubiri iwapo watasonga mbele na azma yao hiyo ya kuchochea mapigano."

Ameongeza kuwa, maadui pia wanalenga kuishinikiza Hizbullah iachana na mpango wake wa makombora yake ya kujihami. Sayyid Hassan Nasrallah amesema hivi sasa Harakati ya Hizbullah ina nukta za nguvu zenye uwezo wa kuainisha hatima na kuongeza kuwa, harakati ya muqawama (Hizbullah) ina uwezo wa kuingia katika eneo la Galilee katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Katibu Mkuu wa Hizbullah katika sehemu nyingine ya hotuba ya amesema hivi sasa imeweza kubainika wazi kuwa Hizbullah ilichukua hatua sahihi katika kuingia vitani nchini Syria. Ameongeza kuwa nchini Syria kulikuwa kunatekelezwa njama ya Marekani na Saudia ambapo natija ya njama hiyo ilikuwa ni kundi la kigaidi la ISIS kuteka asilimai 45 ya ardhi ya Syria. Sayyed Hassan Nasrallah amesema swali ambalo linapaswa kuulizwa ni hili je, ni nani aliyekuwa akiwapa magaidi wa ISIS msaada ya kifedha na silaha nchini Syria na Iraq.

Kiongozi wa Hizbullah amesema ISIS ni kundi la kigaidi linalofuatia itikadi za Kiwahhabi ambalo limeundwa na Saudi Arabia na limekuwa likipokea msaada ya kifedha kutoka kwa utawala huo wa Riyadh.

3808300

captcha