IQNA

Chuo kikuu cha Imam Jafar Sadiq AS

14:04 - August 21, 2014
Habari ID: 1441613
Tarehe 25 Shawwal miaka 1287 iliyopita Imam Jafar Sadiq AS mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW aliuawa shahidi. Alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul na kipindi chake cha Uimamu kilianza mwaka 114 Hijria.

Duru hiyo ya uongozi na Uimamu wake ilidumu kwa muda wa miaka 34 ambapo katika kipindi hicho, Imam Sadiq alifanya hima na idili mtawalia kwa minajili ya kuwaokoa Waislamu na upotoshaji wa kifikra na kidini uliokuwako katika jamii.
Historia inaonyesha kuwa, Ahlul Bayt na Maimamu watoharifu AS walikuja kuendeleza njia ya Bwana Mtume SAW na kuhakikisha kwamba, jamii ya Kiislamu inaishi kwa kuheshimu misingi na matukufu ya Kiislamu. Lengo lao lilikuwa ni kumfikisha mwanadamu katika ukamilifu wa kiroho na kiakhlaqi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Maimamu watukufu walitumia sehemu kubwa ya umri wao kwa ajili ya kuinyanyua jamii kifikra na kiutamaduni na hivyo kumfanya mwanaadamu ajiandalie uwanja mzuri kwa ajili ya maisha ya saada na ufanisi humu duniani na kesho akhera.
Kipindi cha Uimamu wa Imam Sadiq AS ni moja ya vipindi vilivyokuwa vimetawaliwa zaidi na hali ya panda-shuka katika kipindi cha historia ya Uislamu. Katika kipindi hicho, Bani Umaiyyah na Bani Abbas walikuwa wakipambana kwa ajili ya kuwania uongozi. Kwa hakika hitilafu hizo ilikuwa fursa adhimu kwa Imam Sadiq AS ya kuandaa stratejia ya mapambano kwa msingi wa fikra. Katika kipindi hicho, utawala wa ukoo wa Bani Abbas ulikuwa ukitumia hila, hadaa na ahadi za uongo ili kuingia madarakani. Katika mazingira kama hayo, Imam Sadiq AS alifanikiwa kuwakusanya wanafunzi  takriban elfu 4 katika chuo chake kikubwa cha mjini Madina. Wanafunzi hao walikuwa wanatoka katika ulimwengu wa Kiislamu tena wa kaumu na madhehebu tofauti. Elimu mbalimbali zilikuwa zikifundishwa na wanafunzi hao walikuwa wakinufaika na bahari ya elimu ya Imam Sadiq AS. Wanafunzi wengi walifanikiwa kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Imam Sadiq AS mjini Madina, wanafunzi ambao baadaye waliondokea kuwa wasomi waliotabahari na kuwa fakhari kubwa kwa Waislamu ulimwenguni. Wasomi kama Hisham bin al Hakam na Jabir bin Hayyan anayejulikana kama "Baba wa Elimu ya Kemia" ni baadhi tu ya wanafunzi wa Imam Sadiq AS. Mbali na Imam huyo kujihusisha na kulea na kufundisha wanafunzi, alikuwa akiandaa midahalo na mijadala ya kidini baina ya wanafunzi wake na wanafikra pamoja na wasomi wa dini na makundi mengine. Midahalo hiyo kwa upande mmoja ilikuwa ikithibitisha kwamba, haki iko pamoja na maktaba ya Ahlul Bayt AS na kwa upande mwingine ilikuwa ikikuza soko la elimu na maarifa baina ya Waislamu. Hotuba na misimamo ya Imam Sadiq AS ilikuwa ni hoja na ithbati tosha juu ya uhakika huu kwamba, watawala wenye uchu wa madaraka, hawastahiki kuwa viongozi wa jamii ya Kiislamu na kwamba, cheo hiki sio nafasi ya madhalimu na watumiaji mabavu, hasa kwa kuzingatia kwamba, watawala hao madhalimu walikuwa wako tayari hata kupotosha mafundisho ya Mwenyezi Mungu au kuleta bidaa ilimuradi tu wafikie lengo lao hilo. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana Imam Sadiq AS alitumia kila wasaa na fursa iliyojitokeza kwa ajili ya kuwapinga na kuwakataa madhalimu na mataghuti. Mtukufu huyo daima alikuwa akiwatahadharisha wananchi na kuwataka kutowakaribia madhalimu na alikuwa akisema wazi kwamba:
"Kila mtu atakayemsifia mtawala dhalimu na kuonyesha taadhima na unyenyekevu kwake ili aweze kupewa upendeleo fulani, basi mtu huyo atakuwa pamoja na mtawala huyo dhalimu katika moto wa Jahanamu uunguzao."
Imam Sadiq alikuwa akiwatahadharisha wafuasi wake hata kurejea kwa mahakimu wasio waadilifu wa vyombvo vya utawala wa Bani Abbas na alikuwa akiamini kuwa, kufanyia kazi hukumu zilizotolewa na mahakimu hao haijuzu. Siku moja Mansur ad Dawaniqi mtawala katili wa Kiabbas alimuandikia barua Imam Sadiq AS na kumuuliza:
"Kwa nini hufanyi kama wanavyofanya watu wengine ambao wanakuja katika vikao vyetu na kunufaika na sisi?"
Katika jibu lake kwa barua hiyo, Imam Sadiq AS aliandika:
"Sisi hatuna vita vya kimaada ambavyo tunahofia kuvikosa hata tukuogope wewe; na wala huna vitu vya kimaanawi hata tuwe na matumaini na wewe."
Baada ya Mansur ad Dawaniqi kupokea ujumbe huo wa Imam Jafar Sadiq AS naye alimjibu Imam kwa kuandika:
"Basi njoo kwetu na utunasihi."
Imam Jafar Sadiq ambaye alikuwa akitambua vyema malengo machafu ya mtawala huyo dhalimu alimuandikia ifuatavyo:
"Mtu ambaye anatafuta dunia hawezi kukunasihi wewe, kwani dunia yake itakuwa hatarini; na mtu ambaye anatafuta akhera hawezi kuja kwako."
Licha ya kuwa Imam Sadiq AS hakusimama na kuanzisha harakati ya utumiaji silaha dhidi ya watawala mataghuti wa zama zake, lakini alisimama na kupambana nao akitumia silaha ya elimu na kalamu na kila mara alipoingia nao vitani katu hakusalimu amri.
Wapenzi wasikilizaji, kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri na Baraka kwa Waislamu wote ulimwenguni kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Imam Sadiq AS na tunahitimisha kipindi hiki maalum kwa kukunukulieni baadhi ya maneno ya hekima ya mjukuu huyu wa Bwana Mtume SAW.
Imam Sadiq AS amenukuliwa akisema, hakuna wakati ambao ardhi itabakia tupu bila ya kuweko alimu na msomi ambaye watu wanamhitajia na yeye hawahitajii watu hao na yeye yu mwenye kujua halali na haramu.
Aidha amesema, ndugu baina yenu wanahitajia vitu vitatu ambavyo huufanya urafiki wao kudumu na kubakia, kinyume na hivyo hutengana na kuwa maadui. Vitu hivyo ni insafu, upendo na kutooneana husuda.

1441300

Kishikizo: sadiq imam akhera madina
captcha