IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran ina irada na azma ya kuvunja njama za adui

12:51 - February 19, 2015
Habari ID: 2869495
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: “Taifa la Iran daima limeonesha kuwa lina irada imara na lina uwezo na kuvunja njama za adui.”

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran alipoonana na maelfu ya wananchi wa matabaka tofauti wa mkoa wa Azerbaijan Mashariki na sambamba na kuwashukuru na kutoa pongezi zake nyingi kutokana na taifa kubwa la Iran kujitokeza kwa wingi sana katika maandamano ya Bahman 22 (Februari 11, siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) ametoa hotuba muhimu sana na kujadili ndani yake hali ya kiuchumi nchini na vile vile njia za kutatua matatizo yaliyopo hususan udharura wa kutekeleza siasa za uchumi wa kimuqawama; wa kusimama kidete. Aidha ameashiria utunishaji misuli na masharti haya na yale yanayotolewa na Marekani pamoja na vikwazo vipya vilivyowekwa na nchi za Ulaya dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa: Taifa la Iran siku zote limekuwa likithibitisha kwamba lina irada na msimamo thabiti na katika kadhia ya vikwazo pia taifa la Iran linaweza kuvunja njama zote za maadui na kuzifanya zisifanikiwe.
Aidha katika hotuba yake hiyo, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameashiria ripoti zilizotolewa kuhusiana na maandamano ya Bahman 22 zilizoonesha kushiriki kwa wingi mno wananchi kwenye maandamano ya mwaka huku na kupindukia idadi ya walioshiriki kwenye maandamano kama hayo katika miaka iliyopita na kuongeza kuwa: kwa hakika ulimi wangu unashindwa kufikisha inavyotakiwa shukrani zangu nyingi kwa taifa kubwa la Iran kutokana na kujitokeza kwa wingi mno katika maandamano hayo.
Vile vile ameashiria hali ya hewa ya baridi kali na mvua ilivyokuwa katika baadhi ya miji pamoja na tufani ya mchanga huko Ahwaz siku ya Bahman 22 (Februari 11) na kuongeza kuwa: Licha ya hali ya hewa kuwa hivyo na pamoja na kupita miaka 36 ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini mwaka huu wananchi wamejitokeza kwa wingi zaidi, kwa ufanisi zaidi na kwa shauku na hamasa kubwa zaidi ikilinganishwa na huko nyuma na kuyafanya maadhimisho hayo kuwa jambo la aina ya kipekee duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria sababu kuu ya kufanyika kwa ufanisi na kwa uadhama mkubwa maandamano ya Bahman 22 na kujitokeza kwa wingi wananchi katika medani ya maadhimisho hayo na kuchukua wao lijamu ya ufanikishaji wake akiongeza kwamba: Kila wakati ambapo wananchi wanajitokeza katika masuala ya nchi, huwa tunashuhudia miujiza kama hii, na miujiza ya namna hiyo tumekuwa tukiishuhudia siku zote na mara kwa mara humu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa kanuni jumla katika masuala ya kiuchumi na kutilia mkazo ulazima wa kuweko mipango mizuri ya kuwafanya wananchi wajitokeze kwa njia bora zaidi katika masuala ya kiuchumi na kutumia vizuri nafasi na uwezo huo wa wananchi, na baadaye akabainisha sababu zinazopelekea kuwepo matatizo ya kiuchumi akisema: Moja ya sababu kuu za kushuhudiwa hali hiyo, ni mipango ya madola ya kibeberu baada ya vita vya kulazimishwa (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran) madola ambayo yanaendelea kufanya njama za kuikwamisha Iran isije ikawa kambi muhimu ya kiuchumi na kuwa na taathira kieneo na kimataifa.
Ameongeza kuwa: Wamagharibi na hususan Wamarekani wanatumia mbinu mbali mbali kujaribu kuikwamisha Iran katika mipango na harakati zake kubwa za kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kukwamisha ushirikiano wake wa kiuchumi na nchi nyingine za eneo hili na vile vile kuiendea kinyume Iran katika miradi ya mabomba ya mafuta na gesi na njia za ardhini na angani pamoja na kanali za mawasiliano na hususan kadhia ya nyuklia katika miaka ya huko nyuma, ambapo Wamagharibi hao walianzisha vikwazo vya kimya kimya dhidi ya Iran na hadi hivi sasa vikwazo hivyo vinaendelea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: kwa hivyo katika kuyafanyia uchunguzi mazingira na matatizo ya kiuchumi nchini tunapaswa kuizingatia na tusiipuuze mipango ya adui Mmarekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinazoifuata kibubusa Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, inabidi tukabiliane vilivyo na mipango ya wanaolitakia mabaya taifa la Iran kiasi ambacho tutaweza kuzifanya njama hizo za maadui zisiwe na taathira au ziwe na taathira ndogo na kuongeza kwamba: Mbali na kuweko mipango mikubwa na ya kuendelea ya kambi ya kibeberu, uchumi wetu una matatizo mengine mawili makubwa, nayo ni kutegemea kwake mafuta na kuendeshwa kwake na Serikali.
Amesema, kuuza mafuta ghafi na kutumia pato lake katika matumizi ya kila siku ya ndani ya nchi na kutotumia nishati nyinginezo kubwa zinazotokana na bidhaa nyinginezo zitokanazo na mafuta ni urithi mbaya tuliourithi kutoka kwa utawala wa kitaghuti (utawala wa Shah wa kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) urithi ambao una hasara zisizolipizika.
Ameongeza kuwa: Mbinu hiyo ndiyo njia rahisi zaidi ya kupatia pesa na kwamba viongozi wengi wamekuwa wanapenda kutumia sana pesa hizo zinazopatikana kiurahisi kuendeshea mambo ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu matatizo yanayojitokeza wakati uchumi wa nchi unapoendeshwa na serikali na amegusia hatua ya kuwasilishwa siasa kuu za kifungu cha 24 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran miaka michache iliyopita na sisitizo lake la wajibu wa kutekelezwa kivitendo siasa hizo na kuongeza kuwa: Kwa hakika viongozi nchini wanafanya kazi kwa dhati na kwa moyo safi, hata hivyo juhudi hizo hazitoshi na inabidi kufanyike jitihada kubwa zaidi za kukuza uchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja Bahman 29 (Februari 18) kuwa inasadifiana na mwaka wa kwanza wa tangu kuwasilishwa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete nchini Iran na kusisitiza kwamba: Uchumi wa kusimama kidete ni jambo la dharura nchini iwe ni katika mazingira ya vikwazo au nje ya mazingira ya vikwazo. Hii ina maana ya kwamba msingi ya uchumi nchini unapaswa kupangiliwa kwa namna ambayo hautoweza kuathiriwa na mitikisiko ya mara kwa mara inayotokea duniani.
Ameongeza kuwa: Iwapo msingi wa uchumi wa nchi yetu utasimama juu ya uwezo wa wananchi na uzalishaji wa ndani na iwapo kutawekwa mipangilio makini chini ya msingi huo, basi uchumi wetu hautaathiriwa na vikwazo na wala kushuka bei ya mafuta na wala hakutakuwa na wasiwasi wa kuathiriwa na mambo mengine uchumi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja moja ya mambo ya lazima na muhimu ya kuweza kujitoa kwenye uchumi unaotegemea fedha za kuuza nje mafuta kwamba ni kuifanya bajeti ya nchi iache kutegemea fedha hizo za mafuta.
Ameongeza kuwa: Tunapaswa kufikia kwenye nukta hiyo na ninaamini kwamba, kazi hiyo ngumu inawezekana kwa hima na kuwategemea wananchi na vijana pamoja na kutegemea rasilimali na uwekezaji wa za ndani ya nchi na muhimu kuliko yote kumtegemea na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Ambaye ametoa ahadi ya nusra (ya kumnusuru kila anayeinusuru dini Yake).
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa moja ya njia za kuifanya bajeti isitegemee mapato ya fedha zitokanazo na kuuza nje mafuta ni kutegemea fedha zitokanazo na kodi, uzalishaji wa ndani na biashara.
Amesema: Baadhi ya wawekezaji wakubwa ambao wanakwepa na kukimbia kulipa kodi, kitendo chao hicho ni uhalifu kwani kinapelekea nchi kuzidi kutegemea fedha za kuuza nje mafuta na kuandaa mazingira ya kujitokeza matatizo zaidi na zaidi ya kiuchumi.
Amelitaja suala la ulipaji kodi kuwa ni muhimu sana bali ni jambo la faradhi kisheria na kuongeza kuwa: Maafisa wa masuala ya kodi wameweka mipangilio mizuri kwa ajili ya ukusanyaji wa kodi zinazotokana na uzalishaji bidhaa na masuala ya biashara na kwamba inabidi wananchi washirikishwe vilivyo na wasaidie katika ufanikishaji wa haraka mipango hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, nukta nyingine muhimu ya kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi ni kuongeza tija na faida na kuongeza kuwa: Maana ya kuongeza tija ni kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa na wakati huo huo kupandisha juu ubora wa bidhaa hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuweka mipango inayofaa kwa ajili ya kustafidi kadiri inavyowezekana na suhula na uwezo wa vyanzo vya ndani ya nchi kuwa ni njia nyingine ya kuweza kutatua matatizo ya kiuchumi. Baada ya hapo amegusia nukta kadhaa ili kutilia nguvu matamshi yake hayo.
Kustafidi na kutumia bidhaa za ndani ni nukta ya kwanza iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo amesema: Wananchi na watu wote wanaoipenda Iran na mustakbali wa nchi hii pamoja na taasisi zote za kiserikali zinapaswa ziache kutumia bidhaa za nje ambazo bidhaa kama hizo zinazalishwa pia ndani ya Iran.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amebainisha nukta nyingine kuwa ni ulazima wa kujiepusha na israfu na kuzuia kupotea na kutumiwa vibaya mali ya umma pamoja na kuyategemea mashirika ya elimu za kimsingi na kupambana vilivyo na magendo na kuongeza kuwa: Inabidi kazi hizo zifanyike kwa uzito wa hali ya juu ili iwezekane kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi.
Ameongeza kuwa: Katika miaka ya hivi sasa kumetolewa tahadhari na maonyo mengi na kumefanyika jitihada nyingi katika uwanja huo lakini pamoja na hayo maonyo na tahadhari hizo hazitoshi na hata jitihada zilizofanyika hadi hivi sasa ijapokuwa ni nyingi lakini nazo pia hazitoshi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia ulazima wa kulipa umuhimu mkubwa suala la kushirikishwa vilivyo wananchi na uwezo wao katika masuala mbali mbali yakiwemo ya kiuchumi na kuongeza kuwa: Sisi tunao uwezo wa kusimama kidete na kukabiliana na makelele na hatua zinazochukuliwa na maadui kuhusiana na vikwazo na hatimaye kuvivunja nguvu vikwazo hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama hatutachukua hatua zinazotakiwa na kufanya jitihada kwa nguvu kubwa zaidi katika masuala ya kiuchumi, basi matokeo yake yatakuwa ni yale yale ambayo tunayaona hivi sasa ambapo adui anaweka masharti haya na yale katika kadhia ya nyuklia na baadaye anasema kijeuri kwamba kama hamtokubali masharti yetu basi tutakuwekeeni vikwazo.
Vile vile ameashiria namna kambi ya kiistikbari na kibeberu inavyotumia kadiri inavyoweza silaha ya vikwazo dhidi ya taifa la Iran na kusisitiza kuwa: Lengo kuu la maadui kwa hatua yao hiyo ni kulidhalilisha taifa la Iran na kuikwamisha harakati adhimu ya taifa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya kuelekea kwenye ustaarabu mpya wa Kiislamu na mimi ninaamni kwamba, kata kama itatokezea tukakubaliana na matakwa yao katika kadhia ya nyuklia, vikwazo havitaondoshwa kwani maadui hao ni wapinzani wakubwa wa asili ya Mapinduzi yenyewe ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uwezo mkubwa sana walio nao vijana wa Iran hususan wanachuo mabasiji katika masuala ya nchi na katika kufanikisha wa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuashiria vitisho vinavyotolewa na dola la kibeberu na kiistikbari la Marekani pamoja na vikwazo vipya vya nchi za Ulaya dhidi ya Iran na kuongeza kuwa: Kama suala hapa ni kuwekeana vikwazo basi taifa la Iran nalo linao uwezo wa kuweka vikwazo na litafanya hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Taifa la Iran lina irada na azma thabiti sana na kwamba wakati wowote Jamhuri ya Kiislamu inapoingia katika jambo fulani, huonyesha kivitendo azma na nia yake ya kweli na isiyotetereka.
Amesema hatua ya Iran ya kukabiliana vilivyo na kundi la Daesh ni moja ya mifano ya azma yake hiyo kubwa na isiyotetereka na huku akigusia uongo na ubazazi unaotumiwa na Marekani na waitifaki wake katika kudai wanapambana na kijikundi hicho cha kigaidi amesema kuwa: Wamarekani waliiandikia barua wizara yetu ya mambo ya nje na kutwambia kuwa hawaliungi mkono kundi la Daesh lakini siku chache baadaye kulisambazwa picha zinazoonesha namna Marekani inavyolisaidia kijeshi kundi hilo la Daesh.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia sehemu nyingine ya hotuba yake kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya hamasa ya wananchi wa Tabriz ya Bahman 29 mwaka 1356 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Februari 18, 1978 Milaadia) na kulitaja suala la kuzijua vizuri zama, nyakati na kuchukua hatua wakati unaofaa, ushujaa na imani ya kweli kuwa ni katika sifa za kipekee za wananchi wa Azerbaijan na wa mji wa Tabriz katika nyakati tofauti na amemtaja kwa wema Ayatullah Mohammad Mojtahed Shabestari mwanachuoni mwana jihadi ambaye ana busuri na anaangalia mambo kwa mtazamo wa mbali.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, wananchi ndio wamiliki halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu na nchi ya Iran na mwishoni mwa hotuba yake amesema kwa kusisitiza kwamba: Ni jambo lisilo na shaka kuwa, taifa la Iran litafikia vilele vya vya juu vya heshima na fakhari katika mustakbali usio mbali sana.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mojtahed Shabestari, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyul Faqih) katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki ambaye pia ni Imam wa Sala ya Ijumaa wa mji wa Tabriz ametoa hotuba fupi na sambamba na kuashiria hamasa kubwa iliyooneshwa na taifa la Iran katika maandamano ya Bahman 22 (Februari 11 mwaka huu) amesisitiza kuwa: wananchi wenye ghera na uchungu wa Azerbaijan wana historia ya kujitokeza vilivyo katika nyuga mbali mbali nyeti kwenye historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na hususan katika harakati yao ya Bahman 29, 1356 (Februari 18, 1978) na katika kulinda umoja wa ardhi yote ya Iran na kufanikisha ushindi wa mapinduzi matukufu ya Kiislamu.
Mwakilishi huyo wa Fakihi Mtawala katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki ameongeza kuwa: Wananchi wenye welewa mpana wa Azerbaijan kutokana na uwezo na suhula za aina yake walizo nazo katika upande wa elimu, viwanda na kuheshimu matukufu ya Kiislamu, mara zote wako mstari wa mbele kwenye jitihada za kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu.../mh

2865269

captcha