IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu: Muqawama usio na kifani Gaza umeutukuza Uislamu

13:21 - March 27, 2024
Habari ID: 3478588
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, Muqawama (mapambano ya Kiislamu) usio na kifani wa vikosi vya Muqawama na watu wa Ghaza umeutukuza Uislamu.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo katika mkutano na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS pamoja na ujumbe aliofuatana nao.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Jumanne jioni jijini Tehran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuenzi muqawama na kusimama imara kusio na mfano kwa vikosi vya Muqawama wa Palestina na watu wa Ghaza na kusisitiza kuwa, subira ya kihistoria iliyoonyeshwa na watu wa Ghaza mbele ya jinai, unyama na ukatili wa utawala wa Kizayuni unaofanywa kwa uungaji mkono kamili wa Magharibi ni jambo adhimu mno ambalo kwa hakika limeutukuza Uislamu; na kinyume na matakwa ya adui, limeligeuza suala la Palestina kuwa suala kuu la ulimwengu.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, mauaji ya watu wa Ghaza na mauaji ya kimbari yanayofanywa katika eneo hilo yanamuathiri kila mwenye hisia za utu na akaongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita hata chembe kuunga mkono kadhia ya Palestina na wananchi wake wa Ghaza wanaodhulumiwa na waliosimama imara.

Vile vile ameienzi kumbukumbu ya shahidi Al-Arouri, mmoja wa viongozi wa Hamas ambaye aliuliwa shahidi na utawala wa Kizayuni, na akasema: "Shahidi huyu mtukufu alikuwa shakhsia mashuhuri ambaye hatima yenye baraka ya kufa shahidi ndiyo tuzo aliyomlipa Mwenyezi Mungu kwa juhudi nyingi za Jihadi alizofanya".

Katika mkutano huo, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Hamas sambamba na kutoa shukurani na kuthamini uungaji mkono wa wananchi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kadhia ya Palestina hususan wananchi wa Ghaza aliwasilisha kwa Kiongozi Muadhamu ripoti kuhusu matukio ya karibuni yaliyojiri katika medani ya mapambano na katika uga wa kisiasa ya vita vya Ghaza na akasema: subira na istiqama ya kupigiwa mfano iliyoonyeshwa na watu wa Ghaza na vikosi vya Muqawama katika miezi hii sita, ambayo imetokana na imani yao thabiti, vimemfanya adui Mzayuni ashindwe kulifikia hata moja kati ya malengo yake ya kimkakati katika vita vya Ghaza.

Sambamba na kusisitiza kuwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa imefuta ngano na dhana kwamba utawala wa Kizayuni haushindiki na kwamba baada ya kupita miezi sita adui Mzayuni amepata hasara kubwa na maelfu ya askari wa utawala huo wameuawa na kujeruhiwa, Haniya ameongeza kuwa: vita vya Ghaza ni vita vya dunia na uongozi wa Marekani ni mshirika mkuu wa jinai zinazofanywa na Wazayuni kwa sababu ndio uliobeba dhamana ya kuongoza moja kwa moja vita vya utawala wa Kizayuni.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas amemhakikishia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba licha ya unyama, mauaji ya kimbari na jinai zote zinazoendelea kufanywa huko Ghaza, wananchi wa Ghaza na vikosi vya Muqawama wamesimama imara na hawataruhusu adui Mzayuni afikie hata chembe ya malengo yake.

4207249

Habari zinazohusiana
captcha