IQNA

Mwanazuoni wa Lebanon

Umoja wa Waislamu ni njia pekee ya kukabiliana na maadui

16:31 - November 02, 2020
Habari ID: 3473320
TEHRAN (IQNA) – Mwanazuoni wa ngazi za juu nchini Lebanon amesema umoja wa Waisalu ni sera bora zaidi katika kukabiliana na maadui wanaouhujumu Uislamu na kuvunjia heshima matukufu yake.

Katika mahojiano maalumu na IQNA kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Muqawama, Sheikh Maher Hammoud amesema migogano na ukosefu wa umoja miongoni mwa Waislamu ni chanzo cha maadui kutawala.

"Iwapo Waislamu wataungana kiukweli, basi utawala wa Israel hautathubutu kukalia tena kwa mabavu ardhi za Palestina, na Marekani haiwezi kuthubuti kupora mafuta na utajiri mwingine wa nchi za Asia Magharibi au kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo."

Aidha amesisitiza kuwa, iwapo Waislamu wataungana, madola ya kiistikbari duniani, mabebeberu na maadui wengine katu hawataweza kutawala nchi za Waislamu.

Halikadhalika Sheikh Hammound amesema umoja utaziwezesha nchi za Kiislamu kuchukua hatua za maendeleo na ustawi wa kasi.

Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaamini kuwa Mtume Muhammad SAW alizaliwa 12 Rabiul Awwal nao Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kuwa ni 17 Rabiul Awwal.

Kwa msingi huo, Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya Umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa Waislamu kote duniani.

Kwingineko katika matamshi  yake, , Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Muqawama, Sheikh Maher Hammoud amesema Waislamu wanapaswa kuchukua hatua ya pamoja kukabiliana na vitendo vya hivi karibuni vya kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu.

Amesema hivi karibuni Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah alipendekeza kuchukuliwa hatua ya kisheria dhidi ya wanaouvunjia heshima Uislamu, wazo ambalo pia limeungwa mkono na Imamu wa Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri na wanazuoni wengine duniani.

Sheikh Hammound pia amesema hatua ya rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuunga mkono wale wanaovunjia heshima matukufu ya Kiislamu na hasa Mtume Muhammad SAW, ni hatua ambayo inatekelezwa kwa amri ya Wazayuni.

3932444

captcha