IQNA

Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Mkutano wa 37 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu Iran

19:48 - October 01, 2023
Habari ID: 3477676
TEHRAN (IQNA)- Kongamano la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu limeanza leo jijini Tehran kwa hotuba ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Hujjatul Islam Hamid Shahriari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu, ambaye  aliwasilisha ripoti kuhusu programu za mkutano huu

Wageni wa mkutano huo ni wanazuoni, wasomi na wanaharakati 110 kutoka nchi 41 na pia wasomi wa hapa nchini Iran.

Mwaka huu, zaidi ya makala 200 kutoka nchi 20 kama vile Misri, Algeria, Tunisia na Iraqi katika lugha tofauti zimetumwa kwa sekretarieti ya mkutano.

Kutokana na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya na idhini au kimya cha viongozi wa nchi husika, mwaka huu yatafanyika maonyesho ya Qur'ani Tukufu pambizoni mwa Mkutano wa Umoja wa Kiislamu, na madhumuni ya maonyesho haya ni kutambulisha sura ya rehma ya Uislamu kwa ulimwengu.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu Iran hufanyika katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama siku za Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

3485381

Habari zinazohusiana
captcha