IQNA

Sayyed Hassan Nasrallah

Ujerumani imeshindwa kuthibitisha madai yake dhidi ya Hizbullah

19:05 - May 05, 2020
Habari ID: 3472735
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amelaani hatua ya Ujerumani ya kuiita harakati hiyo kuwa eti ni kundi la kigaidi, na amesisitiza kuwa serikali ya Ujerumani imeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha madai yake.

Sayyid Hassan Nasrallah alisema hayo jana Jumatatu katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja na televisheni ya Al Manar na kueleza bayana kuwa: Uamuzi huo wa Ujerumani ulitarajiwa kwa kuwa umechukuliwa kwa mashinikizo ya Marekani.

Amesema harakati hiyo ya muqawama itaendelea kusimama kidete dhidi ya uvamizi na chokochoko za utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kulilinda taifa la Lebanon.

Kadhalika Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amezishukuru nchi na serikali za dunia ambazo zimetoa taarifa za kulaani hatua hiyo ghalati ya Ujerumani ya kulinasibisha harakati hiyo ya mapambano na makundi ya kigaidi.

Tangazo hilo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani limekabiliwa na radiamali ya pamoja na mhimili wa muqawama katika eneo hili la Asia Magharibi, huku nchi mbali mbali duniani kama vile Iran, Yemen na Syria zikilaani hatua hiyo.

Uamuzi huo wa Ujerumani umechukuliwa sambamba na hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kuunganisha sehemu ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi unazozikalia kwa mabavu huko Palestina.

3896502/

captcha