IQNA

Waislamu Marekani wapinga ubaguzi, wataka mageuzi idara ya polisi

20:35 - June 16, 2020
Habari ID: 3472871
TEHRAN (IQNA)- Mashirika ya Waislamu nchini Marekani yamejiunga na wimbi la malalamiko ya kuishinikiza serikali ya nchi hiyo ifanye mageuzi haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuondoa ubaguzi wa rangi wa kimfumo katika muundo wa polisi ya nchi hiyo.

Katika taarifa ya pamoja kwa niaba ya Waislamu wa Marekani, mashirika 95 ya kiraia kutoka majimbo 30 ya Marekani yakiongozwa na Chama cha Mawakili Waislamu nchini humo yamesema, "vitendo vya kunyanyaswa na kukandamizwa Waislamu weusi ambao hawana silaha vina historia ndefu ya kutisha."

Mashirika hayo yameeleza bayana kuwa, "sisi kama Waislamu wa Marekani, pasina kujali tofauti zetu za kijamii, tutatumia nguvu zetu na ukakamavu wetu kushinikiza mageuzi haya katika idara ya polisi, kwa kuwa maisha ya watu weusi ni muhimu pia."

Asasi hizo za kiraia za Waislamu wa Marekani zimesema haziwezi kunyamazia kimya jinai hizo za kuchupa mipaka za polisi ya Marekani dhidi ya watu weusi, kwani Waislamu nchini humo wamekuwa wahanga wakuu wa unyanyasaji huo kwa miaka mingi sasa.

Kwa karibu wiki tatu sasa, maandmanao yanaendelea kote Marekani kulalamikia vitendo vya ubaguzi wa rangi vya polisi wa nchi hiyo kufuatia kuuliwa kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika kwa jina la George Floyd. 

Maandamano haya ya kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi yanashuhudiwa pia katika nchi mbalimbali duniani, hususan za Ulaya.

Itakumbukwa kuwa, Mnamo Mei 25, afisa wa polisi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota nchini Marekani alimbinya shingo kwa kutumia goti kwa dakika 9 hivi George Floyd, Mmarekani mweusi mwenye asili ya Afrika hadi akakata roho.

Mauaji hayo ya kinyama yaliibua maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa Marekani kupinga ubaguzi wa rangi huku miito ikitolewa ya kulifanyia marekebisho jeshi la polisi na kuondolewa nembo zote za ubaguzi wa rangi nchini humo.

Pamoja na hayo, Rais Donald Trump wa Marekani amelipongeza jeshi la polisi nchini humo huku akipuuzilia mbali kilio cha waandamanaji ambao wanasema kuna ubaguzi mkubwa katika jeshi hilo.

Katika hotuba yake hivi karibuni, Trump amedai kuwa ni maafisa wachache wabaya katika jeshi la polisi.  Hadi sasa Trump amekataa kuzungumza wazi wazi kuhusu ukatili wa polisi dhidi ya Wamarekani weusi huki akidai kuwa maudhui hiyo si muhimu.

3471717

Kishikizo: waislamu marekani Floyd
captcha